Jumapili 30 Agosti 2026 - 17:22
Taasisi ya “Sadiq al-Amin” Mjini Sidon Yaadhimisha Kumbukumbu ya Kuzaliwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na Imam Sadiq (as)

Hawza/ Katika kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Mtukufu, Muhammad (s.a.w.w.) na Imam Jaafar Sadiq (as), na kwa mnasaba wa “Wiki ya Umoja wa Kiislamu,” Taasisi ya “Sadiq al-Amin” nchini Lebanon imeendesha mkusanyiko wa kiroho na wenye hamasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu, Hadhrat Muhammad (s.a.w.w.) na Imam Jaafar Sadiq (as), na kutokana na mnasaba wa “Wiki ya Umoja wa Kiislamu,” Taasisi ya “Sadiq al-Amin,” kwa ushirikiano na tawi lake la Sidon nchini Lebanon, imeendesha mkusanyiko wa kiroho na wenye hamasa. Hafla hiyo ilianza kwa kuswali Swala ya Jamaa, iliyoongozwa na Mshauri wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hujaatul-Islam Sayyid Muhammad Reza Murtadha, katika mazingira yaliyojaa roho ya mapenzi, upendo na furaha ya tukio hili lenye baraka.

Baada ya kuswali, programu ya maadhimisho ilianza kwa hotuba ya Mshauri wa Utamaduni wa Iran, na baadaye kufuatiwa na mkusanyiko wenye nuru wa kujiunganisha na Qur’ani Tukufu. Katika sehemu hii, aya za Kitabu cha Mwenyezi Mungu zilisikika kwa sauti za wasomaji wa Qur’ani, Hajji Haitham Ayyash na Muhammad Abu Amr, jambo lililoipa hafla hiyo harufu ya unyenyekevu na uzuri wa Qur’ani.

Programu za hafla hiyo ziliendelea kwa hotuba ya Sheikh Khodr al-Kabash, mwanazuoni wa Kisunni nchini Lebanon, na baadaye hotuba ya Sheikh Ahmad al-Zaitouni. Wawili hao walifafanua maana za tukio hili, ishara zake za kiimani na za kuleta umoja, pamoja na maadili mapana na yenye kukidhi nyanja mbalimbali ambayo mwenendo wa Mtume na mwenendo wa mjukuu wake, Imam Sadiq (as), unayabeba kwa ajili ya Umma.

Programu hiyo ilihitimishwa kwa mashindano ya kuhifadhi “As-Siraj al-Munir” (Aya za 40 hadi 48 za Suratul-Ahzab), yaliyofanyika katika kuendeleza mpango wa taasisi wa kuhamasisha kuhifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kujenga uhusiano na Aya za Mwenyezi Mungu. Mwishoni mwa kikao hicho, ambacho kiliunganisha furaha ya Maulid, nuru ya Qur’ani na ujumbe wa umoja wa Kiislamu, zawadi zilitolewa kwa washiriki.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha